Mfanyabiashara tajiri wa New York anayewania urais kupitia chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amepoteza $800m ya utajiri wake katika kipindi cha mwaka mmoja, kwa mujibu wa jarida la Forbes.
Jarida hilo linasema kwa sasa utajiri wa Bw Trump ni $3.7bn (£2.7bn).
Forbes wanasema kushuka huko kwa thamani ya utajiri wake kunatokana na 'kudorora kiasi' kwa biashara ya nyumba na ardhi katika soko la New York.
Bw Trump, ambaye wakati mmoja liandika kitabu kwa jina Midas Touch (Mguso wa Midas: Midas aliaminika kubadilisha kila alichogusa kuwa dhahabu), amekuwa akisema kwamba rais wa Marekani kwa sasa anaweza kuwa mtu mwenye busara katika biashara na majadiliano.
Wakati wa mdahalo wa urais Jumatatu, alisema: "Nina mapato makubwa ... wakati umefika kwa taifa hili kuwa na mtu anayefahamu mengi kuhusu pesa."
Alipoteza vipi $800m?
Forbes, ambao wamekuwa wakikadiria utajiri wa Bw Trumo kwa zaidi ya miongo mitatu, wanasema hilo limetokana na kudorora kwa soko la nyumba, afisi na ardhi New York.
Kati ya majumba 28 ambayo yalichunguzwa na Forbes, 18 yalishuka thamani, likiwemo jumba maarufu la Trump Tower linalopatikana Manhattan.
Jumba lake lililo 40 Wall Street na kilabu chake cha Mar-a-Lago kilichopo Palm Beach, Florida, pia vilipoteza thamani, kwa mujibu wa Forbes.
Lakini majumba saba ya Trump, likiwemo jumba la pili kwa urefu San Francisco, yalipanda thamani.
Ametumia pesa ngapi kwenye kampeni?
Inakadiriwa kwamba amewekeza $50m, pesa zake binafsi, kwenye kampeni kufikia sasa.
Forbes wanakadiria kwamba matamshi yake dhidi ya wahamiaji wa Mexico yalimgharimu $100m kupitia mikataba aliyopoteza kwenye mashirika makubwa kama vile NBC Universal, Univision na Macy's.
Utajiri wake kamili?
Utajiri wake kamili haujulikani. Alipowasilisha taarifa zake za kifedha kwa Tume ya Dola ya Uchaguzi, alisema ana "zaidi ya dola bilioni kumi."
- Akamatwa kwa kupanda jengo kuu la Trump
- Evan McMullin: Mpinzani mpya wa Trump
- Trump: Putin anamshinda Obama kwa uongozi
Lakini Forbes wanasema utajiri wake ni $3.7bn, Bloomberg wanasema anamiliki $3bn nao Fortune wanasema ana $3.9bn.
Moja ya sababu inayochangia hili ni kwamba Bw Trump pia huhesabu thamani ya jina lake, ambalo anakadiria kwamba thamani yake ni karibu $3.3bn.
Post a Comment