Kundi la kigaidi la Boko Haram limetoa kanda ya video, wanayodai inaonyesha wasichana waliotekwa nyara katika eneo la Chibok miaka miwili iliyopita.
Video hiyo, inamuonyesha mwanamume mmoja aliyejifunika uso wake, akiwa amejihami kwa silaha, akizungumza na kundi la wanawake takriban 50.
Wote wamevalia mavazi ya kidini.
Mmoja wa wanawake hao anajitambulisha kuwa, Madia na kusema kuwa anatoka Chibok.
Anasema wenzake kadhaa wamejeruhiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya angani ya wanajeshi wa Nigeria.
Anatoa wito kwa serikali kuwaachilia wanachama wa Boko Haram, ili wasichana hao waachiliwe huru.
Inaonekana kuwa Boko Haram inatumia video hiyo kuwafanya raia wa Nigeria kuwahurumia wasichana hao, na kuilazimu serikali kutimiza matakwa yao.
Serikali ya Nigeria haijasema lolote kuhusiana na video hiyo.
Post a Comment