0
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa Sh milioni 250 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa ajili ya kuchangia kampeni ya madawati Mkoa wa Dar es Salaam. Licha ya kukabidhi msaada huo, mamlaka hiyo pia imechangia Sh milioni 165 katika Halmashauri 11 nchini zenye uhaba wa madawati.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi (TPA), Profesa Ignas Rubaratuka alisema msaada huo ni kutekeleza jukumu katika kuunga mkono kampeni ya Rais John Magufuli ya kuhakikisha wanatatua tatizo la ukosefu wa madawati katika wilaya za mkoa huo ili watoto wa kitanzania wasome katika mazingira bora.
“Pamoja na shughuli zake za kupakua na kupakia mizigo pia mamlaka imekuwa mstari wa mbele kuchangia masuala ya kijamii kupitia sera yake ya msaada kwa jamii ambapo inashiriki kikamilifu kurudisha faida yake kwa jamii,” alisema.
Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo, Makonda alisema msaada huo utasaidia kupunguza uhaba wa madawati zaidi ya 800,000 unaolikumba jiji la Dar es Salaam ambao utasaidia kupunguza adha wanayoipata wanafunzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TPA, Deusdedit Kakoko alisema wameamua kutoa msaada huo lengo ni kurudisha kiasi kwa jamii na msaada uliotolewa umetolewa kwa makubaliano yao pamoja na wafanyakazi wa TPA ili kuondoa uhaba wa madawati katika Mkoa wa Dar es Salaam na Mikoa mingine .

Post a Comment

 
Top