0
Watendaji wa Mkoa wa Pwani watakiwa kuwa wawazi kwa waandishi wa habari pale wanapotaka kupata taarifa kutoka kwao.
Hayo yamesemwa leo Mjini Kibaha, Mkoani Pwani na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura alipofanya ziara ya kikazi mkoani hapo kufuatilia utekelezwaji wa maendeleo ya kisekta kwa wizara yake.
“Kwa kuwapa ushirikiano wakutosha waandishi wa habari kutasaidia kuepuka kuandikwa kwa habari zisizona taarifa kamili ambazo huleta mkanganyiko kwa jamii na kuharibu taswira ya ofisi, hivyo ni vyema mshirikiane nao”,alisema Naibu Waziri Wambura.
Pamoja na hayo Mhe. Naibu Waziri aliangiza kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Kitengo cha Habari kipewe kipaumbele na kitengewe bajeti itakayokidhi mahitaji pamoja na kununuliwa vitendea kazi ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao kwa urahisi ikiwa ni pamoja na kutangaza shughuli za maendeleo ya mkoa.
Kwa upande wa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bw.Shangwe Twamala alisema mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya uhaba wa Maafisa Michezo kwa baadhi ya Wilaya pamoja na Maafisa Utamaduni ila suala hilo kwasasa limeshawasilishwa kwa ngazi husika na wanalifanyia kazi.
Pamoja na hayo Kaimu wa Mkoa huyo aliendelea kusema Mkoa huo unakabiliwa pia na changamoto ya usikivi wa matangazo ya Redio na Televisheni kwa baadhi ya maeneo kama Rufiji,Mafia na mengineyo.
Naye Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Mashariki Bw.Bernard Haule alitoa ufafanuzi kuhusu suala la kukatwa kwa matangazo katika chaneli zote pale malipo yanapoisha katika ving’amuzi vya Azam na Zuku kwa kusema leseni zao ni tofauti na zile za Startimes na Continental ambazo mbali na malipo ya kifurushi yanapokwisha wao bado huonyesha chaneli tano za taifa bure ambazo ni ITV,Star Tv,Channel Ten, EATV na TBC 1.
Pamoja na hayo Mhe.Wambura aliagiza kuwa watendaji wahakikisheni wanatenga maeneo ya viwanja vya michezo yasiyo na mgogoro kwani michezo ni ajira na inasaidia vijana kujikwamua kiuchumi,hivyo ni vyema ipewe kipaumbele.
Halikadhalika Naibu Waziri Wambura alitoa wito kwa wasanii Muziki wa Mkoa wa Pwani kuiga mfano wa marehemu Baraka Mwishehe kwa kutunga nyimbo zenye maadili na zenye kubeba ujumbe wa kuelimisha na kuburudisha jamii.
Hata hivyo Naibu waziri aliendelea kuwasisitiza watanzania wote kwa ujumla kuenzi lugha ya Kiswahili kama yanavyofanya mataifa mengine duniani kuenzi lugha zao mfano China.
PIX 6
Baadhi ya Maafisa Habari,Maafisa Michezo,Maafisa Utamaduni wa Mkoa wa Pwani wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Anastazia Wambura (watatu kushoto) alipofanya ziara ya kikazi leo Mjini Kihaba,Mkoani Pwani kujua maendeleo ya sekta kwa wizara yake , (wapili kushoto) ni Kaimu Mkuu wa Mkoa Bw.Shangwe Twamala na (wapili kulia) ni Mbunge wa Viti Maalum Pwani, Mhe. Hawa Mchafu.

Post a Comment

 
Top