0
Ikiwa imepita siku moja tangu ndege mbili mpya aina ya Bombardier Dash-8 Q400 za serikali kuzinduliwa kwa ajili ya kuanza safari zake rasmi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema safari za ndege hizo zitasaidia kufufua hifadhi za utalii ambazo zilikuwa hazifikiwi kutokana na kukosekana kwa njia rahisi ya kuunganisha safari za watalii.
Waziri Maghembe amezitaja mbuga, ardhi oevu na ghuba zitakazo fufuliwa kuwa ni mbuga za Gombe na Katavi, ghuba za mahale na ardhi oevu ya Kirombelo, ambazo kwa mujibu wa tafiti za kitalii zinaongoza kwa uzuri Afrika na duniani kwa ujumla.
“Ndege hizi zikianza safari zake mbuga nyingi zitafunguka ambazo awali zilikuwa hazifikiwi na watalii kutokana na kutokuwepo usafiri wa uhakika, ” amesema.
Amesema sababu nyengine iliyopelekea vivutio hivyo kutofikiwa na watalii ni gharama kubwa za usafiri.
“Hivi sasa watalii katika baadhi ya maeneo wanatumia dola 1800 kusafiri yaani kwenda na kurudi, mfano kutoka Kilimanjaro kwenda Kigoma watalii wanalipa gharama ya usafiri 1600 kwenda na kurudi hii ni sawa na milioni 4 za kitanzania. lakini kwa sasa watalipa dola 150 pekee, ” amesema.
Maghembe amesema ndege za ATCL zitakapoanza kazi zitasaidia kusafirisha watalii wanaokwenda Zanzibar kwenda katika hifadhi nyingine zilizopo bara kama Serengeti na Manyara kwa sababu utakuwepo usafiri wa uhakika na wa gharama nafuu.
Ametaja hifadhi nyengine itakayonufaika na usafiri wa ATCL ni hifadhi ya bahari ya Marine Park ambayo ni ya 3 kwa ubora duniani.
“Mafia kuna hifadhi ya bahari ilitengenezwa inaitwa Marine Park ni ya tatu kwa ubora duniani lakini ilikuwa haifikiwi na watalii kwa sababu ya kukosekana kwa usafiri wa uhakika, ila kwa ndege hizi kila mtalii atatumia dola 100 kwenda na kurudi,” amesema.

Post a Comment

 
Top