0
Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kuondoa watumishi wote wasiokuwa askari polisi katika idara hiyo.
Magufuli aliyasema hayo baada ya kuwaongoza manaibu kamishna wa polisi 25 na makamishna wasaidizi 35 kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Ikulu Jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli pia ameagiza jeshi hilo lichukue hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha wakiwemo wanaodaiwa kuiba mabilioni ya shilingi zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa sare za askari mwaka jana 2015.
Image copyrightIKULU
Image captionRais Magufuli pia ameagiza jeshi hilo lichukue hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha
"Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, ofisi ya IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) ipo palepale, ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) ipo palepale, Makamishna wote mnazunguka mnakwenda palepale, mwizi mnae palepale, mnashindwa kumshika.
"Kama mnafikiri kuwa na raia katika jeshi la polisi wanawaharibia kazi zenu hamisheni raia wote na wapelekeni utumishi, kwani hakuna mhasibu ambaye ni askari polisi? hakuna mhandisi ambaye ni askari polisi? hakuna afisa tawala ambaye ni askari polisi? Mimi nafikiri kama matatizo ya wizi na wafanyakazi hewa yanaletwa na raia waliomo ndani ya jeshi la polisi na majeshi yetu mengine, IGP kaorodheshe raia wote wanafanya kazi Jeshi la Polisi ili waondolewe na tuwapangie kazi nyingine uraiani" taarifa hiyo ya ikulu ilisema.
Image copyrightIKULU
Image captionMagufuli aliyasema hayo baada ya kuwaongoza manaibu kamishna wa polisi 25 na makamishna wasaidizi 35 kula kiapo cha uadilifu
Magufuli vilevile ametaka viongozi wa Jeshi hilo wawaongoze askari walio chini yao vizuri, wawatie moyo na waache vitendo vya kuwakatisha tamaa kwa kuwaadhibu ama kuwatisha pale wanapochukua hatua stahiki dhidi watu wanaovunja sheria.
"Sasa mimi niwaombe nyinyi, wale wadogo mnaowaongoza mkawape mamlaka ya kutimiza wajibu wao, hata kama ameshika gari la IGP liache lishikwe IGP atakwenda kujieleza mwenyewe, hata akishika gari la RPC afanye hivyohivyo, hata akishika gari la Waziri au gari la Rais mwacheni atekeleze wajibu wake, sheria ni msumeno, tunawanyima nguvu hawa wa chini wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria halafu unamwambia liachie, ukifanya hivyo aliyeshikwa anatoka pale akiwa anatamba kwelikweli na yule askari unamvunja nguvu ya kufanya kazi" Amesisitiza Rais Magufuli.
Image captionMagufuli alionesha ukarimu alipowagawia maafisa hao vitafunia
Rais Magufuli pia amelitaka jeshi hilo kuungana na vyombo vingine vya serikali katika kutekeleza shughuli zake zikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali bandarini, katika sekta ya utalii na maeneo mengine, kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuondoa watumishi hewa.

Post a Comment

 
Top