Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amemteua Jaji Jacob Mwambejele wa Mahakama Kuu-Kitengo cha Biashara kuchunguza mgogoro wa Kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani vya Mfuru, Mbigiri, Mandengwa, Dumila, Matongolo na Maboiga vilivyopo Wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro ili kupata suluhisho la kudumu la mgogoro ambao umedumu kwa miaka takribani 27.
Waziri Lukuvi amemteua Jaji huyo kwa mamlaka yake chini ya kifungu 18 (1) cha Sheria ya Ardhi sura 113.
Uteuzi huo umefanywa leo jijini Dar es Salaam ukiwa ni wa kwanza katika juhudi za utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.
“Huu ni uteuzi wa kihistoria kwani migogoro ya ardhi hapa nchi huwa inatatuliwa kiutawala lakini kutokana na ugumu wa mgogoro huu imebidi nimteue jaji kufanya uchunguzi baada ya kijiji cha Mabwegere kukataa taarifa ya msuluhishi, Bwana Steven Mashishanga,” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, mgogoro huu ni wa muda mrefu tangu 1989 na umesababisha hasara kwa Taifa ikiwemo vifo vya watu, kuua wanyama na uharibifu wa mazao.
Lukuvi amesema kutokana na mgogoro huo kuwa kati ya migogoro mikubwa hapa nchini imebidi jaji ateuliwe ili kufanya uchunguzi ambao utafanikisha kumalizika kwa tofauti hizo.
Jaji Mwambejele ataongoza timu ya watu wanane (8) ambao watafanya kazi ya uchunguzi huko Kilosa Morogoro kwa siku 60, alisema Lukuvi.
Uchunguzi huo utaangalia mambo kadhaa ikiwemo kama uanzishwaji wa kijiji cha Mabwegere ulianzishwa kisheria, kama ulikuwepo usahihi wa kisheria katika upimaji wa eneo hilo na kama wanakijiji walishirikishwa, alisema Lukuvi.
Lukuvi ameyataja maeneo mengine ya uchunguzi huu kuwa ni kuangalia kama upimaji ulizingatia mipaka, kuchunguza maeneo mengine yenye migogoro na kuchunguza jambo jingine lolote ambalo litasaidia katika kuleta suluhu ya mgogoro huo.
Aidha, Lukuvi amewataka watu wa maeneo husika yenye mgogoro kutoa ushirikiano kwa Jaji na timu yake wakati wa uchunguzi ili kuweza kuchangia katika kupata suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Steven Kebwe amemshukuru Waziri Lukuvi kwa hatua aliyochukua kushughulikia mgogoro huo ambao umechukua muda mrefu na kugharimu maisha ya watu na mali zao ikiwemo mifugo na mazao.
“Nitashirikiana na Jaji pamoja na timu yake ili kuhakikisha tunapata suluhu ya mgogoro wa Mabwegere ambao umekuwa ukininyima usingizi,” alisema Dkt. Kebwe.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni Wizara kinara katika kutatua migogoro ikishirikiana na wizara nyingine kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Post a Comment