Mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu kimoja nchini Kenya amejitia kitanzi baada ya kupoteza dau la shilingi 80,000 sawa na dola $800 aliloweka katika mechi za Euro 2016.
Kwa mujibu wa gazeti moja nchini Daily Nation mwanafunzi huyo alikuwa ameweka dau la dola $ 400 kwa ushindi wa Ujerumani na pesa zingine sawa na hizo kwa ushindi wa Italia.
Hata hivyo kinyume na matarajio yake mechi hiyo iliishia sare na kumaanisha kuwa alikuwa amepoteza pesa hizo zote.
Alifunga safari kutoka mjini Nairobi hadi kwao magharibi mwa Kenya alipojitia kitanzi nyuma ya nyumba ya mamake mzazi katika kijiji cha Ondome Uriri jimbo la Nyanza.
Afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo David Kirui anasema kuwa marehemu aliacha ujumbe akisema hakuona haja ya kuendelea kuishi baada ya kupoteza pesa alizopewa za kulipia karo za chuo kikuu.
Ujerumani hata hivyo ilishinda kwa mikwaju ya penalti ilyofuatia.
Ujerumani itachuana dhidi ya wenyeji Ufaransa katika nusu fainali baadaye leo.
Mshindi kati yao atachuana dhidi ya Ureno iliyoizaba Wales mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa jana.
Sasa miapango ya mazishi imeanza huku swala la kuenea kwa michezo ya bahati na sibu ikizua tena mjadala miongoni mwa wapenzi wa kandanda na jamii kwa jumla.
Je kuna njia yeyote ambayo serikali inaweza kuingilia kati ilikuzuia uraibu wa michezo hiyo ya bahati na sibu kugeuka na kuwa karaha ?
Post a Comment