0
Mtoto wa umri wa miezi sita, aliyeokolewa baada ya kukaa kwenye vifusi kwa siku nne, ametambuliwa na kukutanishwa na babake.
Babake mtoto huyo, Bw Ralson Wasike, akihutubia wanahabari, amesema bintiye amekuwa na nguvu sana.
Amesema alikuwa na wasiwasi sana baada ya kumtafuta siku hizo zote na kumkosa.
Msichana huyo alitolewa kwenye vifusi mwendo wa saa kumi usiku na kupelekwa hospitalini kwa mujibu wa maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu.
Alipatikana akiwa amefunikwa kwa blanketi ndani ya ndoo na hakuonekana akiwa na majeraha yoyote.
Huruma
Image captionWatu 22 wamethibitishwa kufariki
Bw Wasike amesema alijawa na furaha sana baada ya kusikia kwamba mtoto huyo alikuwa hospitalini, lakini anasema bado hajafanikiwa kumpata mkewe.
Mtoto huyo ni miongoni mwa manusura waliookolewa baada ya jumba la ghorofa sita kuporomoka katika mtaa wa Huruma, Nairobi baada ya mvua kubwa kunyesha Ijumaa.
Mwingine aliyeokolewa na mtoto wa umri wa mwezi mmoja, kwa jina Joy, aliyetolewa kwenye vifusi saa nane baada ya jumba hilo kuporomoka.
Joy
Image captionMtoto Joy akiwa na mhisani katika kituo cha kuhudumia waathiriwa
Mamake Mildred aliambia BBC kwamba alikuwa na furaha sana kumpata tena mwanawe.
Juhudi za uokoaji bado zinaendelea na watu 95 bado hawajulikani walipo.
Watu 22 wamethibitishwa kufariki.
Wale waliokuwa wakiishi katika jumba lililoporomoka wamejengewa makao ya muda ambapo wanahudumiwa.
Wahisani wanawasaidia kwa chakula na mavazi.

Post a Comment

 
Top