Foleni ndefu zimeshuhudiwa katika vituo vya kupigia kura nchini Zambia ambapo wapiga kura wanashiriki uchaguzi wa urais na wabunge.
Kumekuwa na ushindani mkali na kipindi cha kampeni kilikumbwa na vurugu.
Ushindani mkubwa unatarajiwa kuwa kati ya Rais Edgar Lungu wa chama cha PF na mgombea wa upinzani wa chama cha UPND Hakainde Hichilema.
Kuna jumla ya wapiga kura 6.7 milioni waliojiandikisha kupiga kura.
Kwa mara ya kwanza, mgombea urais anatakiwa kupata asilimia 50 ya kura zitakazopigwa pamoja na kura moja zaidi ili kuepusha awamu ya pili ya uchaguzi.
Bw Lungu alishinda uchaguzi mkuu uliopita kwa kupata 48% ya kura.
Waangalizi wa uchaguzi huo wanasema suala ya kudorora kwa uchumi litakuwa muhimu katika uamuzi wa wapiga kura.
Kuporomoka kwa bei ya shaba nyekundi, tegemeo kuu la uchumi wa taifa hilo, kumesababisha kufungwa kwa migodi na maelfu ya watu kupoteza kazi.
Ukuaji wa uchumi umepungua kwa nusu na serikali ya nchi hiyo iliomba usaidizi wa kifedha kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Isitoshe, sawa na nchi nyingine za kusini mwa Afrika, Zambia imekumbwa na ukame mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 35.
Edgar Lungu alishinda uchaguzi uliofanyika kufuatia kifo cha rais Michael Sata
Chama cha UPND (United Party for National Development) kimemtuhumu Rais Lungu kwa kusimamia "kusambaratika" kwa uchumi.
Lakini chama tawala cha PF (Patriotic Front) kinasema kina mpango wa kutafuta njia mbadala za kukwamua uchumi.
Shirika moja lilionya kwamba ghasia ambazo zimeshuhudiwa baina ya makundi pinzani ya kisiasa wiki za hivi karibuni huenda zikawafanya baadhi ya watu kutojitokeza kupiga kura.
Shirika hilo la Zambian Elections Information Centre linasema wahusika wamekuwa pia hawatii amri ya maafisa wa usalama.
Hakainde Hichelema ameahidi kusimamia vyema uchumi iwapo atashinda.
Jumanne, mkuu wa tume ya uchaguzi Esau Chulu, aliwahimiza wagombea wawili wakoo kutochochea uhasama.
Upigaji kura utamalizika saa 18:00 saa za huko (16:00 GMT) na matokeo yanatarajiwa baadaye Ijumaa au Jumamosi.
Post a Comment