0
UONGOZI wa Simba, mashabiki na wanachama wa timu hiyo jana walifanya usafi kwenye barabara ya Msimbazi yalipo makao makuu ya klabu hiyo kongwe, ikiwa ni moja ya shamrashamra za kuadhimisha tamasha la ‘Simba Day’.
Simba imekuwa ikifanya tamasha hilo Agosti 8 ya kila mwaka ambapo huanza kwa huduma za kijamii kabla ya kumaliza kwa kucheza mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa ambapo pia hutumia nafasi hiyo kwa kutambulisha kikosi na benchi lake la ufundi kwa mashabiki wao.
Kesho tamasha hilo litahitimishwa kwa mechi dhidi ya KMC ya Kinondoni.
Awali akizungumza kabla ya kuanza zoezi hilo mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa jimbo la Ilala, Idd Zungu aliipongeza Simba kuwa na utaratibu wa tamasha ambalo huanza kwa kufanya shughuli za kijamii kila mwaka.
"Kwanza nawapongeza kwa kuacha shughuli zenu na kuitikia kauli ya Rais John Magufuli ya kufanya usafi lakini pia ninyi ni klabu ya kwanza hapa nchini kuwa na utaratibu huu," alisema Zungu.
Zungu akishirikiana na Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, Katibu wa Simba, Patrick Kahemele na baadhi ya viongozi wa matawi ya Simba waliwaongoza wanachama na mashabiki wa Simba kufanya usafi kuanzia makutano ya barabara ya Uhuru na Msimbazi hadi kituo cha Polisi cha Msimbazi.
Mashabiki hao walionekana kuwa na ari huku mara kwa mara wakisikika kusema mabadiliko na wengine kuitikia Moo.

Post a Comment

 
Top