0
Je, wajua kwamba Morocco huwa si mwanachama wa Umoja wa Afrika? Taifa la Morocco linapatikana barani Afrika lakini lilijiondoa kutoka kwa muungano huo zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Morocco ni taifa la Kiarabu lakini nusu ya raia wake huzungumza lugha ya Kiberber au Kifaransa kama lugha mama.
Wakati mmoja, taifa hilo lilitaka kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Mfalme Hassan wa Morocco wakati mmoja aliwahi kusema Morocco ni kama mti wenye mizizi yake Afrika na matawi yake Ulaya.
Mwaka 2000, mrithi wa Mfalme Hassan, wakati wa ziara yake Ufaransa, Mfalme Mohammed VI, afahamikaye sana miongoni mwa raia wa Morocco kama M6, alihimiza uhusiano mpya baina ya EU na Morocco na nchi nyingine za kaskazini mwa Afrika.
HassanImage copyright
Image captionMfalme Hassan alisema mizizi ya Morocco imo Afrika na matawi Ulaya
"Baada ya kukubaliwa kwamba Uturuki inaweza kujiunga na EU, basi suala la Morocco kujiunga na EU si mwiko tena,” alisema msemaji wake Hassan Aourid.
Lakini wakazi wengi wa Ulaya bado walikuwa wanashangazwa na uwezekano wa kuwa na taifa la Kiislamu katika kundi la mataifa yanayotazamwa kuwa ya Kikristo.
Sababu kuu ya Morocco kujiondoa kutoka kwa Umoja wa Afrika ilikuwa hatua ya muungano huo kutambua jimbo la Sahara Magharibi ambalo kwa kirefu linafahamika kama Saharawi Arab Democratic Republic (RASD) kuwa mwanachama wa muungano huo ambao wakati huo ulijulikana kama OAU.
Jimbo hilo huwa linataka kujitenga kutoka kwa Morocco.
Morocco huchukulia jimbo hilo kuwa sehemu ya ufalme wake na inasisitiza kwamba hilo haliwezi kupingwa.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukijaribu kutafuta suluhu tangu 1991 baada ya mkataba wa kusitisha vita kutiwa saini na kukomesha vita vilivyoendelea tangu 1975 Morocco ilipotwaa eneo hilo lililotawaliwa awali na Uhispania.
Morocco kwa sasa imekuwa ikitaka kurejea AU na imekuwa ikifanya juhudi za kudiplomasia kuwashawishi viongozi wa mataifa ya Afrika kuikubali.
Waziri wa mambo ya nje ya Morocco Salahedine Mezouar amezuru mataifa mengi ya Afrika yakiwemo Misri, Libya, Sudan, Senegal, Tunisia, Cameroon, Cote D’ivoire na Ethiopia katika kinachoonekana kuwa juhudi za kutaka kuungwa mkono.
MarrakeshImage copyrightAFP
Image captionMji wa Marrakesh nchini Morocco
Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye kwa atakuwa mwenyekiti wa mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika utakaofanyika Jumapili na Jumatatu mjini Kigali alizuru Morocco Juni 20-21.
Rais Kagame alifanya mashauriano na Mfalme Mohammed VI mjini Casablanca, ingawa haijabainika iwapo suala la Morocco kurejea AU lilijadiliwa.
Mei 2015, Waziri wa mambo ya nje wa Senegal Mankeur Ndiaya alisema AU haijakamilika bila Morocco.
Morocco inataka ruhusiwe kurejea bila masharti, jambo ambalo linaibua maswali kuhusu mustakabali wa jimbo la Sahara Magharibi.

Post a Comment

 
Top