Msimu mpya ligi Kuu ya England unaanza rasmi kesho. Wachambuzi wengi wa soka wanabashiri msimu huu kuwa na msisimko wa aina yake, ambao pengine haujawahi kuonekana.
Timu kadhaa 'vigogo' zimepata mameneja wapya na ambao sifa zao katika ufundishaji na kusaka ushindi hazihitaji maelezo yoyote ya ziada.
EPL katika historia yake ya miaka 24 haijawahi kushuhudia mameneja wenye sifa za kimataifa wakikutana na kukabiliana uwanjani katika ligi moja. Hii ni mara ya kwanza.
Pep Guardiola, wa Manchester City, rekodi yake akiwa Barcelona na Bayern Munich 'inatisha'.
Aliyoyafanya Antonio Conte wa Chelsea akiwa na Juventus si ya kawaida na hata kushangaza wengi katika Euro 2016 akiwa na timu ya taifa ya Italy.
Jose Mourinho, hatimaye akiipata kazi aliyokuwa 'akiiota' kwa miaka mingi, ametua Old Trafford, na licha ya baadhi ya wadadisi kuhoji mikakati yake, sifa yake ya kupata ushindi inafahamika.
Jurgen Klopp wa Liverpool ambaye soka lake la kupeleka wapinzani mchakamchaka kwa dakika zote tisini litakumbukwa tangu akiwa na Borussia Dortmund.
Hawa ni baadhi ya makocha wapya katika baadhi ya zile 'top four', lakini kuna sura mpya pia kama vile Sunderland (David Moyes), Everton (Ronald Koeman), Southampton (Claude Puel), Swansea (Francesco Guidolin), Watford (Walter Mazzarri), na West Ham (Slaven Bilic). Ingawa wengine wana uzoefu kiasi wa EPL.
Na kuna wakongwe wa EPL, - Tony Pulis (West Brom), Mark Hughes (Stoke City), Alan Pardew (Crystal Palace), wakiongozwa na - Arsene Wenger.
Kwa miaka mingi, ligi ya England, licha ya kutotabirika kwake, (Leicester ni mfano hai wa hivi karibuni) imekuwa na timu kadhaa zinazojulikana kama 'top four', na baadhi zikin'gan'gania katika eneo hilo kwa muda mrefu huku nyingine zikiibuka na kuchukua nafasi ya timu zinazoonekana kufifia au kupoteza mwelekeo.
Ligi yenye purukushani
Katika msimu huu mpya, hata wachambuzi wazoefu wa ligi hii yenye 'purukushani' wanashindwa kutaja bayana 'top four', kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya mameneja wapya na jinsi walivyofanya usajili wao, au mipango ya usajili, kwani dirisha bado li wazi hadi mwisho wa mwezi huu.
Nimekuwa likizo ya wiki mbili (bila shaka mashabiki wa soka waliliona hilo kutokana na kutoweka kwa tetesi za soka), na katika siku mbili zilizopita nimepata muda wa kutembelea vilabu kadhaa vya EPL, na kusikiliza hisia za mashabiki kuhusiana na msimu huu mpya, na wengi wanasubiri kwa hamu na hasa kuona mpambano wa mameneja wanaowika Ulaya, na mameneja ambao wanaibuka na filosofia ya soka la kisasa.
Mfano mzuri wa mameneja wapya wanaoibukia ni Eddie Howe, 38, meneja wa Bournemouth.
Kuna baadhi ya magazeti Uingereza hata yametoa tetesi kuwa huenda hata akatua Emirates, iwapo 'Profesa' ataamua kuondoka msimu ujao mkataba wake utakapomalizika.
Eddie Howe amefanya kazi kubwa katika klabu hiyo na ufundishaji wake una 'pumzi' mpya inayoashiria kwamba kandanda inabadilika, na vijana kama yeye wanaona inapoelekea.
Mwingine bila shaka yoyote ni Mauricio Pochettino. Ushahidi ni jinsi alivyoibadilisha Tottenham, kiasi kwamba msimu uliopita timu hiyo ya kaskazini mwa London hata ilithubutu kuanza kuota ndoto za ubingwa.
Hata Argentina ilifikiria kumtaka akafundishe timu ya taifa. Si kazi ndogo, mameneja hawa wapya ndio kizazi kijacho cha kuakisi akina Alex Ferguson na Mzee Wenger, na watataka kuonesha uwezo wao.
Kuelezea matarajio ya msimu huu natumia msemo ulioingia hivi karibuni nchini Tanzania- ligi msimu huu itakuwa ya "mwendo kasi".
Tumeona majina mapya, ya mameneja na hata wachezaji wakiwasili katika ligi tajiri zaidi duniani, ambayo pia imevunja rekodi ya dunia ya usajili.
Bila shaka yoyote, kitimtim kitakuwa si cha kawaida. Na BBC Ulimwengu wa Soka itakuwa ikikuletea matangazo ya moja kwa moja, kila wiki ya Ligi Kuu ya England.
Jumamosi tutatangaza mechi kati ya Hull City wakianza na mabingwa watetezi Leicester City. Jumapili tutakuwa Emirates, Arsenal wakicheza na Liverpool.
Panapo majaaliwa utakuwa nami na Said Sultani Thani, na Israel Saria. Lakini pia ningependa kusikia kutoka kwako, Je 'top four' msimu huu itakuwa nani na nani? Au sasa imefika 'top six'? Tafadhali Unipe na sababu za kufanya utabiri wako. Tweets kama kawa @salym
Shukran sana.
Post a Comment