0
MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Simba, Laudit Mavugo amesema amekuja kwenye timu hiyo kulipa deni kwani Wanasimba wana moyo wa uvumilivu.
Mavugo ambaye alikuwa akicheza Vital 'O ya Burundi, alitua Dar es Salaam wiki hii na juzi alianza mazoezi na timu hiyo tayari kwa msimu mpya wa Ligi Kuu 2016/2017.
"Sikutaka kusaini Vital'O kwa vile nina deni Simba tangu mwaka jana, nimekuja kuwalipa kwani watu wa Simba ni wavumilivu sana wangeweza kunishtaki lakini hawakufanya hivyo watulie nimekuja kuwafanyia kazi," alisema Mavugo.
Mavugo anatarajia kutambulishwa kwenye tamasha la Simba kesho na atakuwa anavalia jezi namba 45. Naye Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, baada ya mazoezi alisema Mavugo ni mchezaji mzuri na anajua anachokifanya.
“Ni mchezaji mzuri na kwa mazoezi ya leo (juzi) amenivutia naamini atakuwa mshambuliaji tishio,” alisema Omog.
Kabla ya kuja Simba, Mavugo alikwenda kufanya majaribio Ufaransa lakini alipofika walimtaka akae kwenye kituo cha kukuza vipaji ili ajifunze soka la kimataifa kwa mwaka mmoja bila mshahara badala ya kufanya majaribio kama walivyokubaliana wakati anaenda na kuamua kurudi kwao.

Post a Comment

 
Top