WAKATI suala la serikali kuhamia mkoani Dodoma likiwa dhahiri zaidi kila siku moja inayoongezeka, Rais John Magufuli ametangaza kuuza majengo ya wizara Dar es Salaam, mara atakapohamia yeye katika makao makuu hayo ya nchi.
Akizungumza
jana kwenye mkutano wa hadhara mkoani Singida, katika siku ya kwanza ya
ziara yake itakayomfikisha mikoa minne, Rais Magufuli alisema
atahakikisha anauza baadhi ya majengo hayo kwa mnada, ili wale wasiotaka
kuhama, wahame kwa lazima.
Mbali
na Singida, mikoa mingine atakayotembelea katika ziara hiyo aliyoanza
jana ni Tabora, Shinyanga na Geita, ambako atazungumza na wananchi
katika mikutano ya hadhara.
Katika
mikutano hiyo, Rais Magufuli anatarajiwa kushukuru wananchi kwa
kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, na kueleza juhudi
zinazofanywa na serikali kutatua kero zao na kuwaletea maendeleo.
Majengo mazuri
Katika
tangazo hilo, Rais Magufuli amesema majengo atakayoanza nayo, ni yale
yanayotazama bahari; ambayo ndiyo mazuri zaidi, yenye mwonekano mzuri
kutoka ofisini.
“Atakayeng’ang’ania
kubaki huko, ajue hana kazi wala mshahara. Hatuwezi kuendelea kukaa
miaka hamsini tunaimba tu kuhamia Dodoma, wakati hatutekelezi uamuzi
wetu hadi wengine wameshatangulia mbele za haki,” alisema.
Alisema
anajua akiitisha zabuni ya ofisi hizo, wateja watayakimbilia kwa wingi,
hivyo wataong’ang’ania kubaki Dar es Salaaam, watakuwa wamejifukuzisha
kazi wenyewe.
Uamuzi
huo wa serikali kuhamia Dodoma japo ni wa siku nyingi na utekelezaji
wake ulikuwa ukifanyika kidogokidogo kwa baadhi ya wizara na ofisi nyeti
kujenga majengo yake katika mji huo, lakini hivi karibuni umepata kasi
ambayo haijawahi kupatikana, baada ya Rais Magufuli kutangaza
kuhakikisha serikali yote inahamia Dodoma kabla ya 2020.
Tamko
hilo la Rais Magufuli lililotolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM wiki
iliyopita na kurejewa katika Sikukuu ya Mashujaa mwanzoni mwa wiki hii,
liliungwa mkono mara moja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye
alitangaza kuharakisha umaliziaji wa ujenzi wa nyumba yake, ili ahamie
katika mji huo Septemba mwaka huu.
Wizara zenyewe
Baadhi
ya mawaziri waliohojiwa na vyombo mbalimbali vya habari, walikaririwa
wiki hii wakisema kuwa suala hilo halina mjadala ni la kutekeleza mara
moja.
Mbali
na waliohojiwa, mawaziri na watendaji wakuu wengine serikalini,
walitangaza muda maalumu kwa watendaji wao kuanza kuhamia katika mkoa
huo.
Miongoni
mwa mawaziri hao, ni pamoja Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk
Charles Tizeba, ambaye naye wiki hii alikutana na vyombo vya habari na
kutangaza kuwa baadhi ya watendaji wa wizara hiyo, wataanza kuhamia
Dodoma kuanzia wiki ijayo.
Dk Tizeba alikaririwa akisema tayari watendaji wa wizara hiyo wanaotakiwa kuhamia Dodoma wameanza kufanya maandalizi ya safari.
Wakati
Tizeba akitajwa kuwa waziri atakayewahi kuhamia pamoja na wizara yake
Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin
Ntalikwa, naye alitaja utaratibu wa kuhamia Dodoma.
Profesa
Ntalikwa aliwataka wakuu wa idara na vitengo wote wa wizara hiyo,
kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma na kuwa wametekeleza agizo hilo
ifikapo Septemba, mwaka huu, muda ambao Waziri Mkuu naye anatarajiwa
kuwa Dodoma.
Agizo
hilo la Wizara ya Nishati na Madini, liliwekwa katika waraka uliotolewa
na watendaji na nakala yake kutumwa pia kwa Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Madalali viwanja
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana jana alipiga marufuku uuzaji
wa viwanja ndani ya mji wa Dodoma, baada ya kubaini kuwepo kwa kundi la
madalali kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo kutoka Dar es Salaam kuhamia
katika mji huo.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari Rugimbana alisema amepiga marufuku
uuzaji huo mpaka baada ya siku 14 baada ya Waziri Mkuu kuhamia Dodoma,
wakati Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), ikishirikiana na kikosi
kazi kilichoundwa na serikali chini Ofisi ya Waziri Mkuu, watakapotoa
utaratibu.
Alisema
kumezuka kundi la madalali kutoka mikoa mingine walioanza biashara ya
viwanja na mashamba bila kufuata utaratibu na kanuni, hivyo uongozi wa
mkoa wamezuia suala hilo, kwani linaweza kuvuruga na wananchi watakaotoa
viwanja kwa madalali hao itakuwa imekula kwao.
Lengo
la serikali kwa mujibu wa Rugimbana, ni kuhakikisha kila Mtanzania
mahali alipo anaweza kupata kiwanja huko alipo. Rugimbana alisema mji wa
Dodoma ulipangwa siku nyingi; kila eneo na matumizi yake ya ardhi hivyo
kuwataka wanaotaka kununua ardhi kuwa makini, ili wasiuziwe maeneo ya
makaburi au masoko.
“CDA
watafanya kazi vizuri na Mtanzania yeyote anayeweza kununua eneo huko
alipo bila ya kuja Dodoma na atakuja hapa wakati wa kukabidhiwa hati na
kiwanja,” alisema.
“Ndani
ya siku 14 tutatoa maelekezo namna ya kupata viwanja Watanzania wawe
watulivu utaratibu mzuri unakuja na hakuna Mtanzania ambaye anataka
kujenga Dodoma atakosa kiwanja.
“Mtu anayetaka, asubiri na mfumo utakuwa wazi kwa kila mmoja na utaratibu wa kisheria utafuatwa,” alisema.
Miji miwili
Pamoja
na hayo Mkuu huyo wa Mkoa alisema baada ya wizara mbalimbali kuhamia
Dodoma, maeneo ya mjini yatakuwa kwa ajili ya biashara na mji wa
serikali utakuwa kuanzia Ihumwa hadi Chamwino Ikulu ambapo zitajengwa
ofisi za serikali.
Kuhusu
ofisi zitakazotumiwa na wizara mara baada ya kuhamia Dodoma mwaka huu,
Rugimbana alisema watatumia ofisi zilizopo mjini kabla ya ujenzi katika
eneo la Ihumwa ambako kutakuwa na ofisi hizo za muda.
‘’Wizara
zikija Dodoma zitaanza kutumia ofisi zilizopo ambazo zilikuwa
zikitumika awali kabla ya ujenzi wa ofisi katika eneo la Ihumwa
kukamilika,’’ alisema.
Alisema sababu ya kupeleka mji wa kiserikali Ihumwa, ni kuondoa msongamano wa magari kama ilivyo katika jiji la Dar es Salaam.
Alifafanua
kuwa kutakuwa na miji miwili; mji wa serikali utakaokuwa Ihumwa na mji
wa kibiashara utakaokuwa katika Mji wa Dodoma. Aliwatoa hofu watumishi
wa wizara mbalimbali watakaohamia Dodoma kuwa kuna nyumba za kutosha za
wao kuishi.
‘’Dodoma tuna nyumba nyingi sana, watumishi hawawezi kukosa nyumba, tutawakodishia hata nyumba binafsi ili waishi,’’ alisema.
Post a Comment