0
SIKU chache baada ya uteuzi wa wakuu wa wilaya, Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania limeeleza kufurahishwa na namna Rais John Magufuli anavyozidi kujipambanua kwa Watanzania kuwa Rais wa Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa.
Katibu wa Jukwaa hilo, Mtela Mwampamba akizungumza Dar es Salaam jana alisema uteuzi wa wakuu wa wilaya umezingatia uadilifu, uwajibikaji, uzalendo na uwezo wa kiongozi husika katika kuwaunganisha wananchi.
“Jukwaa linatumia fursa hii kumpongeza Rais kwa uteuzi wa wakuu wa wilaya alioufanya hivi karibuni. Rais amezidi kudhihirisha kuwa yeye ni kiongozi anayeishi na kusimamia kile anachoahidi kwa vitendo.
“Rais alisema na namnukuu; ‘Nimeona vijana ndio wachapakazi, wasiopenda rushwa na wazalendo, hivyo nitaendelea kuwaamini ndani ya serikali yangu kwa kuwateua kunisaidia kazi mbalimbali’, mwisho wa kunukuu.
“Hili amelitimiza na kulithibitisha katika uteuzi huu wa wakuu wa wilaya ambapo kwa zaidi ya asilimia 70 ya wateuliwa wote ni vijana. Sote tunajua vijana wana ari, utayari na shauku ya kuongoza kwa sifa ya kiuongozi ambazo ni uadilifu, ubunifu, uwajibikaji na uzalendo."
Alisema jukwaa hilo linatoa rai kwa Watanzania, viongozi wa dini na kisiasa kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli katika harakati za kuleta maendeleo.

Post a Comment

 
Top