Klabu ya Saudi ya Al-Qadisiyah FC, imempa ruhusa mchezaji kutoka Ivory Coast Hervé Guy kuondoka klabu hiyo kwenda kupokea matibabu baada ya madaktari kuwashauri kutomtumia kiungo huyo wa kwa sababu anaugua maradhi ya moyo.
''Madaktari walituonya kutomtumia Herve kwenye mechi baada ya uchunguzi wa madaktari kuonyesha kwamba mchezaji huyo anaugua maradhi ya moyo,'' Mkurungezi wa Al-Qadisiyah Ghazi Aseri aliambia vyombo vya habari nchini humo.
''Tumemruhusu asafiri nje ya nchi hii ili aweze kupokea matibabu zaidi.'' Aseri ameongezea.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33, alijiunga na Al-Qadisiyah mapema mwaka huu baada ya kuhama kutoka katika timu ya Ittihad Tanger ya Morocco ambapo aliwachezea kwa miaka minne.
Mapema mwaka huu nyota wa Ivory Coast Cheick Tiote alizimia na kufariki muda mfupi baadaye wakati wa mazoezi kutokana na kinachodhaniwa kuwa maradhi ya moyo akiwa na klabu yake ya China.Alikuwa kwenye kikosi kilichoshiriki michuano ya Kombe la Dunia la vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2003 na alianza uchezaji wa kulipwa katika timu ya Bastia ya Ufaransa na kuelekea Ivory Coast na kujiunga na klabu ya Stella ya d'Adjamé.
Al-Qadisiyah, amesema wataimarisha kikosi chao na amesisitiza wataendelea kumuunga mkono Herve Guy kwa wakati huu.
''Tutaongeza mchezaji mwengine katika kikosi chetu kwani Herve anahitaji muda wa kupona.
''Hatutamuondoa kabisa kutoka kwa kikosi chetu bali tunamuunga mkono na tunamtakia afueni ya haraka,'' Ghazi Aseri amesema
Post a Comment