Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) amesema mahakama hiyo imeanzisha uchunguzi wa awali kuhusu mauaji ambayo yamekuwa yakitokea nchini Burundi.
Bi Fatou Bensouda amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu matukio Burundi tangu Aprili 2015 na kwamba amara kwa mara amezitaka pande zote husika kutojihusisha na ghasia na amauaji.
“Nimekuwa nikiwatahadharisha kwamba wale wanaodaiwa kuhusika katika mauaji yanayoshughulikiwa na Mahakama ya ICC wanaweza wakawajibishwa,” amesema kupitia taarifa.
“Afisi yangu imetathmini mawasiliano na ripoti kadha za mauaji, kufungwa, kuteswa, ubakaji na aina nyingine za udhalilishaji wa kidogo pamoja na watu kutoweka. Hivi vyote vinaonekana kuwa chini ya makosa yanayoangaziwa na ICC.”
Watu 430 wameuawa na wengine 3,400 kukamatwa tangu kuanza kwa machafuko Aprili mwaka jana.
Machafuko hayo yalitokana na hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kwamba angewania urais kwa muhula watatu.
- Pikipiki zapigwa marufuku Bujumbura
- Milipuko ya guruneti yatokea Bujumbura
- Annan: Nkurunziza hakustahili kuwania urais
Baadaye mwezi Mei kulitokea jaribio la mapinduzi ya serikali ambalo halikufua dafu.
Bw Nkurunziza aliwanua urais na kushinda mwezi Julai.
Uchunguzi wa awali hutumiwa na ICC kubaini maelezo yaliyopo ili kuamua iwapo kuna msingi wa kutosha wa kufanya uchunguzi kamili.
Bi Bensouda amesema afisi yake itawahusisha maafisa wa serikali ya Burundi kwa lengo la kujadili na kutathmini uchunguzi na uendeshaji wa kesi katika ngazi ya kitaifa.
Burundi ni mwanachama wa ICC na ilijiunga rasmi na mahakama hiyo Desemba 2004.
Post a Comment