Kampuni ya vinywaji vya Coca Cola imelazimika kulifanyia mabadiliko tangazo lake la biashara linalofahamika kama "Taste the feeling" kufuatia kuingiliwa kati na bodi inayodhibiti filamu nchini Kenya.
Bodi hiyo ambayo awali imelaumiwa kwa kukiuka mipaka yake, ilitangaza leo asubuhi kuwa Coca Cola italifanyia mabadiliko tangazo hilo kwa misingi ya kimaadili.
Mkurugenzi mkuu wa bodi ya filamu ya bodi hiyo nchi Kenya Ezekiel Mutua, alisema kuwa tangazo hilo lilikosolewa na umma kutokana na picha za kubusiana ambazo zinatajwa kuwa za kukiuka maadili ya kijamii.Mutua amesema kuwa baada ya kufanya mkutano na meneja wa Coca Cola nchini Kenya Nicholas Mruthu , kampuni hiyo imekubali kuleta tangazo lingine lisilo na picha kama hizo.
Bodi hiyo pia imeonya makampuni ikiyataka yaheshimu maadili ya familia kutokana na kile yanayojumuisha kwenye matangazo ya biashara na muda ambao matangazo hayo yanapeperushwa .
Post a Comment