0

Cruz ameshinda upande wa Republican, naye Sanders akashinda Democratic
Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Ted Cruz ameshinda mchujo wa chama hicho katika jimbo la Wisconsin, hilo likiwa pigo kubwa kwa Donald Trump.

Katika chama cha Democratic, Bernie Sanders alipata ushindi mkubwa dhidi ya Hillary Clinton anayeongoza kwa wajumbe kwa sasa.

Bw Trump anaongoza kwa wajumbe na katika kura za maoni chama cha Republican, lakini kuna wasiwasi kwamba huenda akashindwa kupata wajumbe wa kumuwezesha kuidhinishwa moja kwa moja kuwa mgombea.

Wapinzani wa Bw Trump wanatumai kwamba hilo likifanyika basi wanaweza kubadilisha mambo katika mkutano mkuu wa chama hicho wa kuidhinisha wagombea mwezi Julai.

Katika mkutano huo, iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya nusu ya wajumbe, ni viongozi wa chama ambao watakuwa na usemi katika kuamua mgombea.

“Leo ni siku muhimu sana, inatoa ujumbe kwa watu wa Marekani,” Bw Cruz amewaambia wafuasi wa chama hicho Milwaukee.

“Tunashinda kwa sababu tunaunganisha chama cha Republican.
Bw Cruz huenda asipate wajumbe wa kutosha kumuwezesha kushinda uteuzi moja kwa moja, lakini viongozi wa chama cha Republican wanamuunga mkono katika juhudi za kumzima Bw Trump.

Bw Trump kwa upande wake amesema kwamba ana matumaini kwamba atafanikiwa licha ya kushindwa Wisconsin na akamshambulia mpinzani wake.

"Ted Cruz ni mbaya kushinda kikaragozi, yeye ni kama kirusi, anatumiwa na viongozi wa chama kutupokonya uteuzi,” maafisa wa kampeni wa Bw Trump wamesema kupitia taarifa.

Viongozi wa chama wana wasiwasi kwamba Bw Trump hatakuwa na nguvu sana katika kukabiliana na mgombea wa Democratic uchaguzini iwapo ataidhinishwa na pia kwamba anaweza kuathiri wagombea ubunge wa Republican uchaguzini.

Kura za maoni zinaonesha hapendwi na wanawake, watu wa Hispania na vijana.
Katika upande wa Democratic, ushindi wa Sanders jimbo la Wisconsin umemuongezea nguvu kabla ya mchujo muhimu New York na Pennsylvania.
Sanders na Clinton ndio pekee waliosalia chama cha Democratic
Seneta huyo wa Vermont, akiwahutubia wafuasi wake Wyoming, amesisitiza kwamba kampeni yake inaendelea kushika kasi na kwamba atabadilisha mambo.

"Mabadiliko kamili huwa hayafanyiki kutoka juu kwenda chini, huwa yanatoka chini kwenda juu,” amesema.

Bi Clinton yuko mbele sana kwa wajumbe na wadadisi wengi wa kisiasa wanasema ana uwezekano mkubwa wa kushinda uteuzi wa chama cha Democratic licha ya kushindwa majimbo kadha karibuni.
Ingawa Bw Trump alishindwa mchujo huo wa Jumanne Wisconsin, bado ana muda wa kujikwamua.

Post a Comment

 
Top