Mwanaume mmoja Mchina alipigwa na butwaa alipokwenda kuomba cheti cha nidhamu kwa polisi na kugundua kuwa 'alinyongwa' miaka 10 iliyopita!
Mtu huyo anayejulikana kwa jina moja tu Chen aliachwa kinywa wazi alipojipata katika orodha ya wale waliokufa.
Chen mwenye umri wa miaka 45 aliviambia vyombo vya habari kuwa daftari maalum ya serikali ilimuoredhesha kuwa alinyongwa mwaka wa 2006 kwa makosa ya kumteka nyara mtu na akahukumiwa kinyonga!
Chen alikuwa amepata kazi mjini Guangzhou na alihitaji cheti cha kudhibitisha kuwa alikuwa na nidhamu nzuri kabla ya kupewa kazi.
Hata hivyo upekuzi uliofanywa na waandishi habari wapekuzi wa kituo cha runinga cha Guangdong uligundua kuwa kulikuwa na mtu mwenye jina hilo na nambari sawa na zake za kitambulisho aliyehukumiwa kifo.
Chen aliwashangaza wengi alipoelezea jinsi maisha yake yamekuwa shwari hadi hapo alipojipata ''mfu kwa muongo mmoja''
''Mimi hata nilipata cheti cha kusafiria kwenda Hong Kong na Macau sijawahi kushuhudia kitu kama hichi maishani mwangu.''
Maafisa wa polisi katika jimbo la Guangzhou walikiri hitilafu hiyo na kumpa cheti alichohitaji iliaendelee kusukuma gurudumu la maisha.
Masaibu ya Chen ni mfano tu ya baadhi ya makosa katika daftari la watu nchini China ambayo yameruhusu watu kupewa vitambulisho vilivyotolewa tayari.
Hata hivyo wizara ya usalama wa umma unasema kuwa hiyo ni hitilafu ambayo inaendelea kusahihishwa katika kampeini iliyoanza mwaka wa 2009.
Mwaka huo kulikuwa na watu milioni moja waliokuwa wakitumia vipande bandia bila kujua.
Post a Comment