0
Wakala wa Vipimo Tanzania imewafungulia kesi mahakamani wafanyabiashara saba waliokuwa wakifanya uchakachuaji wa mizani za kupimia Pamba ambapo kati ya kesi hizo nne zimetolewa hukumu na wafanyabiashara hao wamelipa faini na zilizobakia ziko mahakamani.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Elimu, Habari na Mawasiliano wa Wakala wa Vipimo (WMA), Irene John alipokuwa akieleza hatua zilizochukuliwa hadi sasa baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakulima wa pamba hususani kanda ya ziwa.
Bi.Irene amesema kuwa kila ukifika msimu wa pamba wanunuzi hao hutumia mizani iliyochakachuliwa na kuwaibia wakulima na hivyo msimu huu ulivyoanza wakatuma maofisa wao katika vituo vyote vinavyonunua pamba ili kuhakikisha uuzaji wa pamba unafanyika kwa kutumia vipimo sahihi kwa lengo la kumlinda mkulima na katika ukaguzi huo wamefanikiwa kukamata wafanyabiashara hao wasio waaminifu.
Aidha amesema kuwa kabla ya kutuma wataalamu wake, wakala wa vipimo(WMA) ilituma wataalaumu wake kuzunguka mikoa yote inayolima pamba hususani Kanda ya Ziwa ili kutoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara kuacha udanganyifu huo kwani unaathiri sekta nzima ya kilimo hicho.
Aliongeza kuwa uchakachuaji huu umeifanya pamba ya Tanzania kila inapofika katika soko la dunia kushushwa bei kwa kukosa ubora ukilinganisha na zamani ambapo pamba ya Tanzania iliitwa dhahabu nyeupe kwenye soko la dunia na kuchukua alama ya kwanza kwa ubora wa pamba yetu, hivi sasa hali imebadilika baada ya kuzuka mchezo huo michafu.
Kaimu Meneja uyo wa Elimu,Habari na Mawasiliano amewaasa pia wakulima kuacha mtindo wa kuweka maji, mchanga na hata mawe ili kupata kilo nyingi katika pamba kwani vinaathiri mbegu na hivyo kupotea thamani ya zao lenyewe na kuhaidi zoezi hili la ukaguzi litaendelea mpaka msimu wa pamba utakapoisha mwezi wa nane.
Aidha amesema kuanzia mwaka huu adhabu ya uchakachuaji wa mzani wa kupimia pamba ni faini ya shilingi elfu 50 au miaka mitatu jela.

Post a Comment

 
Top