0
Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amemchagua Mike Pence kuwa mgombea mwenza, taarifa katika vyombo vya habari Marekani zinasema.
Maafisa wa kampeni wa Bw Trump walipanga atangaze uamuzi wake Ijumaa, lakini hafla hiyo ikaahirishwa kutokana na shambulio la kigaidi lililotokea Nice, Ufaransa.
Duru za karibu zimeambia shirika la habari la ABC News kwamba Bw Pence amekubali kuwa mgombea mwenza.
Hata hivyo, Bw Trump aliambia Fox News Alhamisi jioni kwamba: “Bado sijafanya uamuzi wangu wa mwisho, uamuzi wa mwisho.”
Wachanganuzi wanasema Bw Trump atatumaini bw Pence atamsaidia kuwavutia wahafidhina katika chama chake.
Wagombea wengine ambao walipigiwa upatu kuchaguliwa na Bw Trump kuwa mgombea mwenza ni Spika wa Bunge Newt Gingrich na Gavana wa New Jersey Chris Christie.
Image copyrightAP
Bw Pence ni gavana wa Indiana na mwanachama wa vuguvugu la siasa za mrengo wa kulia la Tea Party.
Akiteuliwa, basi Bw Pence atakuwa makamu wa rais wa Bw Trump iwapo atafanikiwa kumshinda mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton kwenye uchaguzi mkuu Novemba.

Post a Comment

 
Top