0
WASHAMBULIAJI wawili wa Yanga wako hatarini kukosa mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Medeama ya Ghana Jumamosi baada ya kukosa mazoezi kutokana na matatizo tofauti.
Washambuliaji hao, Amiss Tambwe alikosa mazoezi ya juzi baada ya kusumbuliwa na malaria huku Matheo Anthony alishindwa kumaliza mazoezi ya juzi baada ya kuumia.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, Tambwe alikwenda hospitalini kwa matibabu na alitarajia kurejea mazoezini leo kutegemea na hali yake.
Tambwe aliukosa mchezo uliopita dhidi ya TP Mazembe kutokana na kutumikia adhabu ya kadi na huenda pia akaikosa mechi ijayo dhidi ya Medeama kwa sababu ya afya.
Yanga inaendelea na mazoezi Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam huku ikiwa imeweka kambi hoteli ya Ludger Plazza, Kunduchi kujiandaa na mchezo wa tatu wa kundi lake.
Yanga pia itawakosa beki Haji Mwinyi, viungo Deus Kaseke na Geoffrey Mwashiuya katika mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.
Kaseke aliumia kwenye ajali ya pikipiki, wakati Mngwali na Mwashiuya wote wanasumbuliwa na maumivu ya goti na hawataweza kucheza mchezo huo Jumamosi utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga ambayo baada ya kucheza mechi mbili za Kundi A, inashika mkia kwa kutokuwa na pointi hata moja, baada ya kufungwa bao 1-0 na Mouloudia Bejaia ya Algeria Juni 19 na TP Mazembe ya Congo Juni 28.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikaririwa akisema kuwa wanataka kushinda kwa juhudi zote mechi yao hiyo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufufua matumaini ya kucheza nusu fainali.
Cannavaro alisema wamekuwa wakifanya mazoezi kwa juhudi kubwa, pia wanasikiliza kila ambacho makocha wao wanachowaelekeza, kwa kuwa wamelenga kufanya vizuri katika michuano hiyo.


Kocha wa timu hiyo, Mholanzi Hans va der Pluijm alisema kuwa timu yake inaendelea vizuri kupokea mazoezi ya kila siku tayari kuwakabili wapinzani wao hao wa Ghana

Post a Comment

 
Top