0
Mtalii mChina amekamatwa nchini Kenya baada ya kumdunga na kumuua mtalii mwenza vilevile kutoka China katika hoteli moja ya kifahari katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara.
Lee Changqin, ametiwa mbaroni baada ya kumdunga kisu bi Luo Jinli 45 walipotofautiana katika sebule ya mgahawa wa Keekorok.
Changqin alipandwa na hamaki alipowataka marehemu na mumewe Dong Ya kuondoka walikokuwa wameketi wakati wa chajio.
Hata hivyo walimpuuuzilia mbali na ubishi ukazuka ulioishia kwa Changqin kuwadunga wote kisu vifuani.
Kwa bahati mbaya bi Jinli aliaga dunia alipokuwa akipelekwa hospitalini kwa matibabu huku mumewe akilazwa hospitalini katika hali mahututi.
Afisa mkuu wa kitengo cha jinai cha polisi katika eneo hilo Gideon Kibunjah, amenukuliwa akithibitisha kukamatwa kwa bwana Changqin ambaye anasemekana kuwa mzungumzaji mzuri sana wa lugha ya kiswahili tofauti kabisa na wenzake aliowashambulia.
Msemaji wa ubalozi wa Uchina mjini Nairobi amesema kuwa bado hawajapata taarifa kamili kuhusiana na mauaji hayo.
Kenya imeibuka kuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka mashariki ya mbali na haswa Uchina.

Post a Comment

 
Top