0
KATIBU wa chama cha siasa cha ADA-Tadea, John Shibuda amemuunga mkono Rais John Magufuli kwa namna anayojituma kujenga maendeleo na wale wanaomwita mkatili au dikteta, viwango vyao vya kutafsiri ni duni.
Shibuda aliyasema hayo juzi mjini Shinyanga wakati akizungumza na waandishi wa habari, na kutoa mwito kwa vyama vya siasa vya upinzani vijipange upya na kuwa na mtazamo mpya kwa huduma za kisiasa na mashirika ya nje yasiyo ya kitanzania.
Amesema, chama chao kinaunga mkono utendaji kazi wa Rais Magufuli na kwamba wanaomwita katili na dikteta viwango vyao ni duni kwani tafsiri iliyopo kwa wananchi ukatili ni kwa maovu na rafiki wa uadilifu.
“Rais Magufuli ni katili kwa maovu ya kudhulumu haki za wananchi na maendeleo leo ninampongeza kwani ukienda kwenye neno ukatili hata dini zote ni katili zinazodhulumu haki za mwingine kwa kutenda dhambi na kwamba uadilifu ndio utakaowapeleka watu wenye mapenzi ya kweli na peponi, vivyo hivyo namueleza Rais atachukizwa na wapenda maovu nakupendwa na waadilifu,” amesema Shibuda.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini alisema ukweli haulogeki mahimizo ya Rais si udikiteta, bali ni hamira ya kuibua msisimko wa uhuru ni maendeleo na uhuru ni kazi, kwa maana yasiyefanya kazi asinufaike na bofulo la wavuja jasho wenye kupenda kufanya kazi kwa kutii sheria za kikatiba, kanuni na uwajibikaji.
“Hakuna chama kinachotakiwa kufungamana kwa matakwa ya vyama vingine, bali vinatakiwa kuwa na mashirika ya kutaka kukuza ustawi wa maendeleo ya jamii ndio maana chama changu kipo Zanzibar naunga mkono napenda kuwaeleza wanasiasa wawe na matamshi yaliyoshiba mawazo, lishe kwa kuwanufaisha wananchi,” alisema Shibuda.
Alisema Tanzania imo kwenye mfumo wa vyama vingi na ina vyama visiopungua 21 na hakuna chama chochote cha kisiasa ambacho kipo kwa maslahi ya kukweza kingine kwani vyote kazi yao ni kushika hisia za jamii na kutaka kushika dola.
Pia alisema kila chama kina uhuru wa kutafsiri utumishi wa serikali na chama hakuna chama kinacholazimishwa kufungamana na kingine zaidi ya kufungamana na siasa zake zenyewe kwa hiyo sasa vyama vya siasa wasitafute mifereji ya kutotililika minyauko, misinyao za ajenda zenye kuburudisha msukumo wa maendeleo ya wananchi.
Alisema taifa limepata Rais mwenye sifa changamfu za kugusa hisia za jamii, hivyo vyama vya upinzani viwe na mvuto mpya si wa kutengeneza mipasho na vijembe visivyoondoa umasikini na kero katika kaya, bali kuwa kama wanasayansi kila kukicha kubuni mbadala wa tiba na hivyo wanasiasa wabuni ili kwenda na kasi ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Amewaomba wananchi wampongeze Rais kwa kuwatafutia maendeleo na kuwataka wapinzani wasiwe wazibua vizibo vya maovu kwani rais amekuwa akizibua mambo maovu na siyo dikteta, bali mpenda ukweli na mkemea uovu.

Post a Comment

 
Top