JAMIE Vardy anaweza kuwa tayari kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Manchester United utakaopigwa kwenye dimba la Wembley leo.
Mechi hiyo ya kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya England itawakutanisha mabingwa wa kombe la FA ambao ni Manchester United dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya England Leicester City.
Mabingwa hao 20 wa Ligi Kuu ya England wameimarisha kikosi chao kwa kumsajili mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic na kuvutia mashabiki wa timu hiyo.
Mechi za maandalizi za kabla ya msimu za klabu hiyo iliingiliwa na kuahirishwa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya hasimu wao mkubwa Manchester City China na matokeo ya mechi hizo yakiwa mchanganyiko baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Borrusia Dortmund.
Huku ikipata mechi chache kuliko ilivyotarajiwa, kocha wa timu hiyo Jose Mourinho alikiri kuwa atawapa nafasi ya kucheza baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ambao hawakupata nafasi ya kucheza kwenye mechi za maandalizi ya kabla ya msimu.
"Tunaweza kufanya mabadiliko sita badala ya matatu, hivyo hiyo itanipa mimi nafasi ya kutoa muda wa kucheza kwa baadhi ya wachezaji," alisema Mourinho.
"Hiyo itanipa mimi nafasi ya kuchezesha baadhi ya wachezaji kwa dakika 90, kwani hawakuwa na wakati wa kucheza dakika 90," alisema.
Mashabiki wanaitilia shaka Leicester wakati huu wa majira ya joto lakini kocha wa timu hiyo Claudio Ranieri amekataa kupokea mashaka hayo kwamba timu yake haina uwezo wa kukabiliana na presha ya kuwa moja ya timu za juu na anafurahia mtazamo wa kuipa Manchester United nafasi kubwa kwenye mchezo wa leo. Jose Mourinho alikiri kuwa karibu kusajili jina kubwa kwenye nafasi ya kiungo, na kuongeza uvumi wa kiungo Paul Pogba kutua kwenye klabu hiyo.
"Nimesahau kilichotokea msimu uliopita," alisema Ranieri. "Sasa mkazo wangu upo kwenye msimu mpya."
"Hii sio mechi ya kirafiki. Nitaonyesha uwezo wangu wote na Manchester United pia itafanya hivyo-Kila timu inataka kushinda mechi hii."
Claudio Ranieri anaamini mchezaji mpya Bartosz Kapustka anaendana na aina ya uchezaji wa Leicester City na hajaondoa uwezekano wa kufanya usajili mpya kipindi hiki.
Wakati kumkosa N'Golo Kante ni pigo kwa klabu hiyo, kuwabakisha Jamie Vardy na Rihad Mahrez kumewapa matumaini makubwa mashabiki wa timu hiyo na usajili ulioweka rekodi kwenye klabu hiyo wa Ahmedi Mussa anaonekana kuwa kwenye kiwango bora hasa baada ya kufunga bao la uwezo binafsi kwenye kipigo cha mabao 4-2 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Barcelona.
Vardy atafanyiwa uchunguzi wa afya yake kuelekea mchezo huo wa leo. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England alicheza kwa dakika 45 dhidi ya Barcelona akitoka salama na Ranieri anaweka wazi kuwa anaendelea vizuri na mazoezi ya timu hiyo.
Mourinho ana machaguo mengi kwenye safu yake ya ushambuliaji, lakini kuna uwezekano wa kuwapanga Zlatan Ibrahimovic na Wayne Rooney akicheza nyuma ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden.
Bastian Schweinsteiger anaweza kuondoka kwenye klabu hiyo kama sehemu ya mpango wa kocha wa timu hiyo kuijenga timu hiyo. Timothy Fosu-Mensah ni majeruhi wa muda mrefu, lakini Chris Smalling anaweza akacheza sehemu ya mchezo huo akirejea kutoka majeruhi ya misuli.
Takwimu zinaonesha kuwa huu ni mchezo wa kwanza kwa Leicester City wa Ngao ya Hisani tangu mwaka 1971/72 ambapo waliifunga Liverpool kwa bao 1-0. Leicester walikuwa mabingwa wa Ligi Daraja la pili kabla. Huu utakuwa mchezo wa 30 wa Manchester United wa Ngao ya Hisani.Wameshinda taji hilo mara 20.
Ahmed Musa alikuwa nyota wa mchezo kwenye mechi dhidi ya Barcelona akiifungia timu hiyo mabao mawili kwenye mchezo wa kirafiki.
Katika miaka sita iliyopita, Manchester United imeshinda Ngao ya Hisani mara tano(2007/08 na 2008/09 kwa mikwaju ya penalti, 2010/11, 2011/12 na 2013/14).
Mara ya mwisho kwa Leicester kucheza Wembley ni Februari mwaka 2000 ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi Tranmere 2-1. United imeshinda mechi zake nne za mwisho katika uwanja wa Wembley tangu mwaka 2011 tangu ilipofungwa na Barcelona kwenye mchezo wa fainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Post a Comment